Tanzania Network of Legal Aid Providers (TANLAP)

WIKI YA MSAADA WA KISHERIA YAZINDULIWA LEO KARAGWE MKOANI KAGERA

TANLAP kupitia ufadhili wa UN WOMEN leo imezindua wiki ya Msaada wa Kisheria wilayani Karagwe mkoa wa Kagera kuelekea siku ya mwanamke duniani. Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brig. Gen. Marco Gaguti na kuhudhuriwa na Mkuu wa wilaya ya Karagwe, Katika salamu zake, Mkuu wa Mkoa amewasisitiza wananchi wa Karagwe waje kwa wingi kupata elimu ya sheria na kupata huduma ya msaada wa kisheria inayotolewa bure katika viwanja vya Kayanga. Pia amewaasa wananchi kuibua na kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kwenye vyombo husika na kuepuka kujichukulia sheria mkononi. Amewaahidi TANLAP na watoa huduma ya msaada wa kisheria kuwa nao bega kwa bega ili kuhakikisha haki haipindishwi na ipatikane kwa wakati. Viongozi wengine waliohudhuria uzinduzi huo ni Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Kamanda wa Polisi Mkoa, Kamanda wa Polisi Wilaya, Katibu Tawala Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya, Kamanda wa Magereza Mkoa na Wilaya, TAKUKURU Mkoa na Wilaya, Uhamiaji Mkoa na Wilaya, Hakimu wa Wilaya, Mashirika yanayotoa huduma ya msaada wa Kisheria kama MHOLA na wadau wengine wengi . Pia Mkuu wa Mkoa alitumia fursa hiyo kuishukuru UN WOMEN kwa kuendelea kutoa ruzuku za kuusaidia Mkoa wake katika suala zima la elimu ya sheria na huduma ya Msaada wa Kisheria. Pia Afisa Programu wa TANLAP Mr. Mchereli Machumbana alitoa salamu kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANLAP.

Reach Us Today

Biafra/Kanisani, Bwawani Street
Plot No. 434/42, Along Kawawa Road Kinondoni
P.O. Box 33856
Dar es Salaam, Tanzania.
Tel:+255 22 2761806 /0746237265